
Kundi
kubwa la watu watumiaji wa spika ndogo za masikioni (earphone), hasa
wanahabari na wanafunzi, wako hatarini kupata magonjwa mbalimbali
yanayotokana na vijidudu vinavyoambukiza, uchunguzi umebaini.
Uchunguzi
huo umebaini kuwa ni jambo lililozoeleka kwa wanahabari wanapokuwa
vyumba vya habari au maofisini, kuazimana spika hizo bila kuchukua
tahadhari za kiafya.
Mbali
na kundi hilo, kundi kubwa la vijana wadogo, hasa wanafunzi, pia liko
katika hatari ya kupata maambukizo ya magonjwa ya masikio kutokana na
mazoea hayo ya kuchangia matumizi ya spika hizo.
Watu
mbalimbali waliohojiwa, wameelezea kutoelewa athari zinazoweza
kusabishwa na kuchangia earphone ambazo huweza kubeba magonjwa ya ngozi
na yale ya masikio kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine.
Dk
Kareem Segumba alisema uchangiaji wa ‘earphone’ si jambo zuri kwa kuwa
husababisha maambukizi ya magonjwa mbalimbali kutoka kwa mtu mmoja
aliyeathirika kwenda kwa mwingine.
“Kitaalamu tunasema anapata contagious (maambukizi) ya magonjwa ya sikio toka kwa mgonjwa. Magonjwa haya ni pamoja na fungus ya masikio,” alisema Dk Kareem.
Dk
Kareem, ambaye amehudumu katika hospitali mbalimbali nchini, alitaja
magonjwa mengine kuwa ni maambukizi ya sikio sehemu ya mzunguko na
maambukizi kwenye ngoma ya sikio.
“Mara
nyingi mtu anayeumwa fangasi ya sikio au kutokwa na majimaji kidogo
kabla ya kugeuka usaha huwa hawajitambui. Wengi wanajua baada ya kuona
usaha,” alisema.
“Si
desturi nzuri kuchangia earphone na mtu yeyote kwa kuwa madhara yake ni
makubwa na hasa ukizingatia masikio yako karibu sana na ubongo na
huenda ukapata maambukizi kupitia mishipa.
“Mishipa
ya damu inapeleka vijidudu vya ugonjwa kwenye ubongo na hatimaye
kutokea athari nyingine kama uziwi, kupoteza nguvu ya kuona na matatizo
kwenye uti wa mgongo.”
Mpigapicha
wa kituo cha televisheni cha ITV mkoani Kilimanjaro, Robert Minja
alikiri watu wengi hususan wanahabari wamekuwa na tabia ya kuchangia
earphone, kwa vile hawajui madhara.
“Hilo
la ku- share earphone (kuchangia) lipo sana na inavyoonekana watu wengi
hawajui madhara yake. Tunaona ni mambo ya kawaida lakini kiukweli hii
tabia ina madhara ya kiafya,” alisema.
Maulid
Rashid, ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Stefano
Moshi (Smmuco) alisema tatizo la kuchangia vifaa hivyo ni kubwa chuoni
hapo.
“Ni
kweli wanafunzi wengi wanachangia hizo earphone. Nafikiri wanaofanya
hivyo hawana uelewa kuwa kuna madhara. Yaani hili ni tatizo kubwa si kwa
wanafunzi tu hata watu wa kawaida,” alisema.